Friday, May 15

Leo ni Siku ya Familia

Bridgitte akiwa na wazazi wake. Huu ni mfano wa familia katika maana ya zamani, sasa kuna aina nyingi ya familia.
*****

UJUMBE WA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA FAMILIA
15 Mei 2009
Mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Familia inaadhimishwa kwa kauli mbiu isemayo“Akina Mama na Familia: Changamoto Kwenye Dunia Inayobadilika,”Kauli mbiu hii inalenga kuonyesha umuhimu wa akina mama kwa familia na jamii duniani kote.
Akina mama wanatoa mchango mkubwa kwenye familia, mchango ambao unasaidia sana kuleta umoja wa kijamii. Uhusiano kati ya mama na mtoto ni muhimu kwa ukuaji mzuri wa watoto. Na umuhimu wa akina mama sio tu upo katika kuangalia familia; lakini pia katika kutafuta mahitaji kwa ajili ya familia zao. Pamoja na mchango huo akina mama wanaendelea kukumbana na changamoto kubwa, changamoto ambazo wakati mwingine zinatishia maisha yao.
Kwa kawaida, kuzaa mtoto ni tukio la kusherehekewa, lakini kwa wengi kwenye mazingira ya nchi zinazoendelea, uzazi ni tukio linaloambatana na hatari nyingi kwa wanawake. Kuboresha afya ya uzazi ni moja ya malengo ya Milenia. Kwa bahati mbaya hali bado si nzuri. Uwezekano wa mwanamke kwenye nchi inayoendelea kufariki wakati wa kujifungua au kutokana na matatizo wakati wa ujauzito ni mkubwa kwa zaidi ya mara 300 akilinganishwa na mwenzake kwenye nchi iliyoendelea. Ni lazima turekebishe hali hii ili kuhakikisha usalama wa wanawake wajawazito na wale wanaojifungua kwa kuimarisha mifumo ya afya ili itoe huduma za uzazi wa mpango, huduma nzuri wakati wa kujifungua na huduma za dharura za ukunga.
Uonevu dhidi ya wanawake, bado ni tatizo kubwa sana kwa miaka ya sasa. Tatizo hili ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu lina athari kubwa ambazo zinahatarisha maisha ya wanawake na wasichana, kuleta madhara kwenye familia na jumuia zao na kuharibu kabisa msingi wa jamii. Kumaliza na kuzuia vitendo vya uonevu dhidi ya wanawake ni lazima liwe jambo la kipaumbele kwa nchi zote.
Vilevile ni lazima tuhakikishe watoto wote wanakwenda shule. Faida ya kuelimisha wanawake na wasichana haziishii kwa familia tu bali kwa nchi yote. Elimu inasaidia kufungua uwezo uliojificha wa wanawake kuchangia kwenye juhudi za maendeleo. Takwimu zinaonyesha kwamba wanawake waliosoma wana uwezekano mkubwa zaidi wa kusomesha watoto wao. Maana yake ni kwamba faida ya elimu inavuka vizazi.
Wakati tukijitahidi kuwasaidia akina mama kwenye kazi yao ya uangalizi wa familia, ni vizuri pia tukatengeneza na kupanua sera na huduma zinazoendeleza familia kama vile vituo vya kulelea watoto, ambavyo vitawapunguzia akina mama mzigo. Wanawake kama ilivyo kwa wanaume wanahitaji msaada toka kwa jamii ili waweze kusaidiana katika majukumu ya kikazi na kifamilia. Familia zilizojengwa kwa misingi ya kutambua usawa kati ya wanawake na wanaume zinachangia kujenga jamii zenye uthabiti zaidi na zenye maendeleo.
Changamoto ni nyingi kwenye dunia hii inayobadilika, lakini kuna jambo moja halibadiliki: Umuhimu wa akina mama na mchango wao kwenye makuzi ya kizazi kijacho. Kwa kutambua juhudi zao na kuboresha maisha yao, tutakuwa tumejihakikishia mustakabali bora kwa wote.

*****
Nawatakia wadau woote siku njema ya familia, wapendeni watu woote kwenye familia zenu, iwe ni familia ya nyumbani, ya kwako, ya wakwe au aina nyingine.

3 comments:

Anonymous said...

jamani mama x unapenda hii picha, kama hamna zingine si uweke yako, yani nimeiona kama mara 3 hivi sehemu tofauti kwenye hii blog, itakua boring sasa, weka vitu vipya bwana usirudie rudie tena ukiweka latest ni bora zaidi, mana siajabu hata hii ikawa ya mwaka juzi, saizi wameshaongeza na mtoto mwingine

Anonymous said...

ni kweli mama ni kila kitu ktk familia,na ili familia iwe bora mama anaitajika sana na hakuna wa ku-replace kabisa

ashukuriwe muumba kwa kufanya mwanamke-mama

lets be strong n keep our families perfect n happy

shosti jiang uko juu

Anonymous said...

jiang uko busy sana nini............. ok dear keep up the good spirit, fanya kweli weka vitu vipya, vyakutuchamsha usichoke mapema hivi mana ndo blog kwanzaa imeanza