Wednesday, May 19

Michuzi Blog anaahamia .com


Asalaam Aleikhum, Bwana Asifiwe, Tumsifu Bwana, Shalom, Namaste, konnichiwa, Nihao, olá.....
kwa heshima na taadhima nawaamkia  wadau wote popote mlipo ulimwenguni. Salamu nilizotoa hapo juu naomba ifahamike kuwa  hizo nilizozimudu ni kama kielelezo kwamba nia ni kumuamkua kila mmoja kwa nafasi yake popote alipo. Mie sijambo na naendelea na Libeneke kama kawaida.
Waama, baada ya salamu, napenda kuwafahamisha kwamba Globu ya Jamii hivi karibuni itaingia kwenye awamu mpya ya dot com, ikiwa katika jitihada za kuboresha Libeneke zaidi.
Imechukua muda kuchukua hatua hii kutokana na mazoea kwani toka September 8, 2005 hadi leo si kidogo ati. Hivyo mabadiliko kama yapo inabidi yafanywe kwa uangalifu wa hali ya juu ili kutoleta usumbufu wa aina yoyote kwa wadau wa Globu ya Jamii ambao kwangu ndiyo waajiri wangu wakuu.
Naam, wakati wowote kuanzia sasa libeneke la issamichuzi.blogspot.com litaingia katika awamu ya www.imichuzi.com. unakaribishwa kujaribu na kutoa maoni yako.
Mabadiliko haya  tayari yameshaanza na sasa yako katika hatua za nchani. Kilichosalia ni kuhamisha 'mzigo' wote toka issamichuzi.blogspot.com na kuutua katika www.imichuzi.com ili libeneke liendelee vile vile kama siku zote, ukaicha mabadiliko kiasi ya muonekano.
Ni kweli jina litabaki lile lile la 'MichuziBlog' lakini si uwongo kwamba hivi sasa itakuwa tovuti kamili ila  katika sura ya globu kama siku zote. Hii yote ni katika juhudi za kuongeza ufanisi, tija na vionjo vingi zaidi pamoja na kuondoa kero ya kusaka mitundiko iliyopita. Nadhani sasa itaeleweka kwa nini kulikuwa na kwikwi katika kutafuta posti za zamani.
Mdau usihofu kwamba labda utapata shida kusaka www.imichuzi.com. La, hasha. hautopata shida kwani hata kama utaingia Globu ya Jamii kwa kutumia issamichuzi.blogspot.com ama hata kwa kutumia 'michuzi' pekee utapelekwa moja kwa moja kwenye kurasa mpya bila matatizo. Isitoshe, posti zitabakia kwenye ukurasa wa mwezi husika na kuingia kwenye 'archive' baada ya mwezi huo kwisha.
Hivyo basi, kwa unyenyekevu naomba niwashukuru wadau wote popote mlipo kwa kampani yenu wakati wote huu ambayo kwa kweli bila nyie Libeneke lisingefikia hapa lilipo, hususan katika wakati huu wa kulifanya bora zaidi.
Maoni, ushauri na mawazo vinakaribiushwa kwa mikono miwili, pasina kusahau kukosoana kwa kujenga na mawazo mbadala ili kieleweke na Libeneke liendelee mbele.
Kwa kuwa nawapenda wadau wote, nitakuwa mtovu wa fadhila endapo kama sintowaonjesha Libeneke litalokuja kwa muonekano mpya. Hapo hapo naomba radhi kwa usumbufu wowote utaotokea kwani kama inavyofahamika si rahisi kwa binadamu kuwa sahihi kwa kila jambo. Hivyo n penye kwikwi na tusameheane na tushtuane haraka iwezekanavyo kupitia anuani ile ile ya issamichuzi@gmail.com ambayo nayo itabadikika mambo yakikaa sawa muda si mrefu ujao itakuwa info@imichuzi.com

No comments: